¬†Mwinjilisti wa kanisa la African Inland church (AICT) katika kijiji cha Kaseme wilayani Geita, Charles Kazereng’wa amejiuwa kwa kujinyonga baada ya kumuuwa binti yake kwa kumcharaza bakora

Mwinjilisti huyo anadaiwa kumchapa binti yake, Malita Charles (15) akimtuhumu kujihusisha na vitendo vya ufusika.

Inadaiwa kuwa Mwinjilisti huyo alichukua hatua ya kumcharaza bakora bintiye huyo aliyemaliza darasa la saba baada ya kumfuma amesimama barabarani akizungumza na mwanaume.

Tukio hilo lilitokea juzi saa 12:30 jioni katika Kitongoji cha Elimu, Kijiji cha Kaseme wilayani Geita.

Imeelezwa kwamba baada ya kumkuta binti yake katika mazingira hayo, alianza kumcharaza bakora na kwenda hadi nyumbani ambako alimfungia ndani na kuendelea kumuadhibu kwa kipigo hadi alipokata roho.

Bada ya Mwinjilisti huyo kubaini kuwa binti yake amekata roho, aliamua kukimbia na alipofika umbali wa takriban kilomita moja kutoka eneo la tukio, alijinyonga juu ya mti kwa kutumia kamba hadi kufa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Rodson, alithibitisha kutokea kwa matukio yote mawili.

Kamanda Rodson alisema uchunguzi wa kipolisi na kitabibu ukikamilika, miili yote itaruhusiwa kuchukuliwa na ndugu zao kwa maziko.

Akizungumzia tukio hilo, mmoja wa wakazi wa Kata ya Kaseme, Masaga Makanika, alisema limeacha maswali mengi yasiyojibika hasa kutokana na rekodi za marehemu Mwinjilisti Kazereng’wa kuwa muumini mzuri na siku zote amekuwa hana rekodi ya uhalifu.

Chanzo:Nipashe