BOHARI KUU YA DAWA ZANZIBAR YAGAWA DAWA KATIKA HOSPITALI NA VITUO VYA AFYA

0
37

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Afya imesema itahakikisha
kwamba Hospitali na Vituo vyote vya afya vinapatiwa dawa zote muhimu kwa
ajili ya wananchi.

Mkurugenzi wa Bohari kuu ya dawa Zanzibar
Zahran Ali Hamada amesema Serikali tayari imeidhinisha shilingi bilioni
1.6 kwa ajili ya kununulia dawa na Wizara imeshatumia shilingi milioni
600 kununua dawa ambazo zitatosha katika kipindi cha miezi mitatu
ijayo.

Amesema katika mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imetenga
shilingi bilioni tano kwa ajili ya kununulia dawa ambazo zinakidhi
mahitaji ya wananchi katika kuendeleza azma ya Serikali ya kutoa huduma
za afya kwa wananchi bila malipo.

Akisambaza dawa hizo katika
Hospitali na vituo vya afya, Zahran amewaeeleza wafanyakazi kuwa
Serikali imetumia fedha nyingi kununua dawa hivyo amewataka kuzitunza
na kuwapa wananchi kwa mujibu wa mahitaji yao.

“Hakuna haja ya
kuweka akiba dawa wapeni wananchi, dawa zipo zakutosha na utaratibu wa
kuagiza nyengine umeshaanza, ”alisisitiza Mkurugenzi wa Bohari Kuu.

Alisema
Wizara itaandaa utaratibu wa kufuatilia matumizi ya dawa hizo ili
kuhakikisha zinawafikia wananchi na amewashauri viongozi shehia na
wananchi kwa jumla kuwa walinzi wa dawa hizo.

Daktari Msaidizi
wa Hospitali ya Makunduchi Dkt. Asha Salum Hassan amesema hali ya dawa
hivi sasa inaridhisha na dawa nyingi muhimu zinapatikana isipokuwa dawa
za maumivu na Anti biotic zinatumika kwa wingi hivyo baadhi ya wakati
zinakwisha bila ya kuingizwa nyengine. Ameahidi kuwa dawa hizo
zitatumika kama zilivyokusudiwa kwa ajili ya wananchi na atahakikisha
kuwa hakutatokea ubadhirifu wowote ulio nje ya utaratibu uliopangwa na
Wizara.

02
Shehena ya dawa zilizoagizwa na S erikali ya Mapinduzi ya Zanzibar zikiwa zimehifadhiwa kwenye Bohari kuu Maruhubi kabla ya kusambazwa katika hospitali na vituo vya Afya.

03
Wafanyakazi wa Bohari kuu wakisambaza dawa katika Hospitali ya Wilaya Makunduchi ikiwa ni jitihada za serikali kuwapatia wananchi huduma hiyo bila malipo .
04
Mkurugenzi wa Bohari Kuu ya dawa Zanzibar Zahran Ali Hamad akimkabidhi dawa  Daktari msaidizi wa Hospitali ya Wilaya  Makunduchi Asha Salum Hassa (wa pili kulia) kwa ajili ya Hospitali hiyo.

Picha na Makame Mshenga/Maelezo Zanzibar.