HASSANOO, KABURU WAULA TENA CHAMA CHA SOKA MKOA WA PWANI COREFA

0
33

CHAMA cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA) kimepata safu mpya ya uongozi wataoongoza kwa kipindi cha miaka minne ambapo katika   nafasi ya mwenyekiti imekwenda kwa Hassan Hasanoo  baada ya kuchaguliwa kwa kishindo na wajumbe wa mkutano  mkuu uliofanyika katika ukumbi wa kiguza Wilayani Mkuranga.

Katika uchaguzi huo ambao ulikuwa unasubiliwa kwa hamu na shauku kubwa na wadau wa mchezo wa soka ulihudhuriwa  na viongozi wa serikali,viongozi wa michezo kutoka wilaya mbali mbali za Mkoa wa Pwani, waangalizi kutoka shirikisho la soka Tanzania (TFF) wakiongozwa na mkurugenzi wa sheria na wanachama  Eliud Mvella.

Hassanoo ambaye hapo awali alikuwa katika nafasi hiyo ya mwenyekiti ameweza kutetetea kiti hicho kutokana na kuwa mgombea pekee aliyowania nafasi hiyo  baada ya wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kumpigia kura za ndiyo zipatazo 22 katika ya kura 24 zilizopigwa huku akipigiwa kura mbii za hapana.
Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi wa Chama cha soka Mkoa wa Pwani (COREFA) Masau Bwire alisema kuwa nafasi ya Mwenyekiti imenyakuliwa na Hassan Hasanoo aliyepata kura 22 za ndiyo, huku nafasi ya makamu mwenyekiti ikichukuliwa na  Shabani Kangale(Macho kodo) kutoka Wilayani Bagamoyo kwa kujipatia kura 14 dhidi ya mpinzani wake Said Baiza alipata kura tisa.

Kinyang’anyiro kingine  katika uchaguzi huo kilikuwa katika nafasi ya katibu mkuu, ambapo kulikuwa na upinzani wa hali ya juu kutokana na wagombea wote watatu waliokuwa wanaomba kura kuonekana kila mmoja kuwa na dalili za kuondoka na ushindi hivyo kuonekana muda wote wakiwa wana haha uku na kule.

Uchaguzi wa nafasi hiyo ya ukatibu mkuu ilibidi urudiwe kwa mara ya pili kutokana na wagombea wawili kupata kura sawa,ambapo  Robert Mnisi alipata kura (8) Abubakari alawi kura (8) huku aliyewahi kuwa  katibu  mkuu wa  zamani  COREFA Riziki Majala akipata kura 7, hivyo ikamlazimu Mwenyekiti wa uchaguzi kutangaza kurudia upya katika nafasi hizo mbili.

Baada ya uchaguzi huo kurudiwa tena  kwa  mara  nyingine , matokeo yaliweza kubadilika na kuacha midomo ya watu wazi kutokana na mwenendo mzima ulivyokuwa, ambapo Abubakari Alawi aliweza kupata kura 16 na kutangazwa rasmi kuwa katika mkuu, huku mpinzani wake wa awali  Robert Mnisi akipata kura 6 tu huku nafasi ya katibu msaidizi ikienda kwa Godfrey Haule kwa kupata kura 17 za ndiyo.

Katika nafasi ya Mweka hazina alichaguliwa Bernad Yomba Yomba kwa kupata kura 19 za ndiyo, wakati nafasi ya msaidizi wake ikinyakuliwa na Mohamed  Lubondo aliyejizolea kura 21 za ndiyo,kutoka kwa wajumbe wa mkutano  mkuu wa uchaguzi huo.

Makamu wa Rais wa klabu ya soka ya  Simba Godfrey Nyange (Kaburu) aliweza kuitetea nafasi yake ya mwakilishi wa mkutano mkuu wa TFF, baada ya kuweza kupata kura 21 za ndiyo, ambapo Juma Kisomo kutoka visiwani mafia aliweza kuchaguliwa kuwa mwakilishi wa klabu Mkoa baada ya kupata kura zote 24 za ndiyo.

Kwa wa nafasi za wajumbe wa kamati ya utendaji ya COREFA,zilinyakuliwa na Mohamed Mbaruku kura (21) Shaban Mawingu (22) pamoja na mwamuzi mstaafu wa ligi kuu ya Tanzania bara Saimon Mberwa aliyepata  kura zote 24,huku nafasi maalumu ya mjumbe katika soka la wanawake ikinyakuliwa na Frorence Ambonisye kwa kupigiwa kura 23 za ndiyo.
Mwenyekiti mpya wa Corefa Hassan   Hassonoo (mpiganaji) mara baada ya kutangazwa mshindi alitoa pongezi kwa wajumbe wa mkutano mkuu kwa kumchagua tena na kuwahakikishia kwamba atashirikiana nao bega kwa bega katika kuleta mabadiliko chanya katika  kukuza mchezo wa soka katika Mkoa wa Pwani kuanzia ngazi za chini kwa kuanzisha ligi za vijana wadogo .
Mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo mkuu Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya Corefa Masau Bwire aliweza kutumia fursa katika mkutano huo  kutangaza rasmi kustaafu na kuachia nafasi hiyo kutokana na kuchukizwa na baadhi ya watu ambao wamekuwa wakimfanyika fitina , chuki na vitisho  katika kutimiza wajibu wake kulingana na kufuata  kanuni, sheria na taratibu zilizowekwa.