Maria Sharapova apunguziwa adhabu aliyopewa na CAS

0
20

CAS yatoa uamuzi kuhusiana na adhabu ya mwanatenisi wa Urusi Maria Sharapova

Mahakama ya kimataifa ya michezo CAS imetangaza kumpunguzia adhabu Maria Sharapova aliyepigwa marufuku ya miaka 2 kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Kulingana na maelezo yaliyotolewa na CAS, iliarifiwa kwamba mwanatenisi huyo wa Urusi alipunguziwa adhabu yake ya marufuku kutoka miaka 2 hadi miezi 15.

Sharapova alikuwa amewasilisha ombi la kutaka kupunguziwa adhabu hiyo kwa shirikisho la tenisi duniani ITF baada ya kupigwa marufuku ya miaka 2.

Kufuatia uamuzi huo uliotolewa na CAS, marufuku ya Sharapova yatamalizika rasmi tarehe 26 Aprili 2017 na kumwezesha kushiriki mashindano ya taji kuu la Grand Slam la French Open.

Sharapova aliwahi kupewa adhabu hiyo ya marufuku baada ya kufanyiwa ukaguzi kwenye mashindano ya Australia Open tarehe 26 Januari na kugundulika kuwa na dawa za kusisimua misuli.

Sharapova mwenye umri wa miaka 29 alijitetea kwa kusema kuwa hakutambua iwapo kinywaji alichokuwa akitumia kwa miaka 10 kilikuwa na dawa hizo.