Chemical: Sina haraka na mapenzi

0
32

Msanii huyu amekuwa akitamba kwa nyimbo mbalimbali zikiwamo za ‘I am Sorry Mama’, Sielewi, Kama Ipo Ipo tu, VIP Party na Mary Mary’, ambazo zote zimeingizwa kwenye video.

Mwenyewe anasema kwamba nyimbo hizo ameshirikisha wasanii mbalimbali akiwamo Msaga Sumu na zimechangia kumfanya ajulikane zaidi kwa mashabiki wa muziki wa kizazi kipya na kuwa miongoni mwa marapa nyota wa kike nchini.

“Kwanza kabisa mimi ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam niko mwaka wa tatu ninachukua masomo ya sanaa na nilianza muziki mwaka jana nikiwa na wimbo wa Sielewi,” anasema Chemical.

Anasema kuwa katika maisha ana msimamo wake ambao anaamini kwamba unamfanya awe huru na kuepuka usumbufu wa mara kwa mara kutoka kwa wanaume ingawa baadhi ya watu wamekuwa wakimuelewa vibaya.

“Nilishawahi kusema kwamba mimi sijawahi kujihusisha na mapenzi na siyo kwamba sijawahi kutafutwa na wanaume bali nina malengo katika maisha yangu, hivyo siwezi kufanya mambo ovyo tu,” anasema.

Chemical anaongeza kusema: “Ninaamini kwamba mapenzi yapo na wanaume wapo na ninamuomba Mungu nikiwa tayari nipate mwanaume atakayenipenda na kuniheshimu.”

Anasema kuwa kutofanya mapenzi ni maamuzi na mipango aliyojiwekea mtu na haoni kama ni tatizo, ingawa ya watu wamekuwa wakidai kwamba ni msagaji kwa sababu ya kutofanya mapenzi.

“Huo ndiyo msimamo wangu wa kwanza, mwingine ni kwamba katika maisha yangu huwa sitaki vitu vya gharama kubwa kwa ajili ya kujiremba…mimi msichana msomi wa kawaida kabisa na ninaamini nitapata mwanaume anayenipenda jinsi nilivyo,” anasema.

Alisema kuwa anataka jamii imuelewe kwamba hataki kuchanganya mambo katika maisha kwa vile anaweza kujikuta akakwama mbele ya safari ndiyo maana anaona asijihusishe na mapenzi aelekeze nguvu kwenye elimu na muziki wake.

“Nirudie kuwaambia wale wasioamini kwamba mimi sijawahi kufanya mapenzi na wala mimi siyo msagaji bali suala la kufanya mapenzi ni uamuzi kwamba nifanye ama nisifanye, zaidi sana ni kuendekeza tu,” anasema.

Chemical anawataka mashabiki wake waendelee kumuunga mkono katika harakati zake kwenye muziki wa kizazi kipya anazozitoa na kuachana na hao wanaomzushia kuwa ni msagaji.

Anasema kuwa mashabiki ni watu muhimu katika kazi zake kwa vile wanaweza kumshusha au kumpandisha kutegemea na jinsi atakavyowajali ama kuwachukulia kama watu asiowathamini.

Msanii huyu anasema kuwa katika muziki yeye ni mpambanaji ndiyo maana hana muda wa kukimbilia kwenye mambo ya mapenzi ambayo yalianza tangu enzi za Adam na Hawa na bado yataendelea kuwapo tu.

Anasema kwamba sasa ni mwaka mmoja tangu ajitose kwenye muziki huo na kufanikiwa kutangaza jina lake vizuri, hivyo hana budi kuendelea kulifanya liwe juu zaidi kwa kuandaa nyingi zenye ubora.

Kimwana huyu anasema kuwa njia pekee ya kufikia anakotaka ni kutochanganya mambo na kujikuta akikwama baadaye, ndiyo maana anashikilia msimamo wake wa kutojihusisha na mapenzi.