Mahakama Kuu yazuia polisi Tanzania kumkamata Freeman Mbowe

0
58

Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam imewaamuru maafisa wa polisi kutomkamata Mwenyekiti Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) nchini Tanzania, Freeman Mbowe, hadi Ijumaa.


Mkuu wa Jeshi la Polisi  nchini Tanzania ,IGP Ernest Mangu 

Freeman Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Chadema alikuwa amefika katika mahakama hiyo kufuatilia mwenendo wa kesi ya kikatiba aliyoifungua dhidi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Simon Sirro na Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Camilius Wambura.

Katika kesi hiyo, mbali na mambo mengine, Mbowe anapinga amri ya Makonda ya kutaka akamatwe na pia kile alichokiita kudhalilisha watu wakati mkuu huyo wa mkoa alipotaja majina ya watu wanaodaiwa kuhusika katika ulanguzi na matumizi ya madawa ya kulevya.

Mahakama imeliambia jeshi la polisi nchini Tanzania kwamba, linaweza kumuita Freeman Mbowe kwa mahojiano kama litaona umuhimu wa kufanya hivyo, lakini hawaruhusiwi kumkamata.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) anayepingwa na baadhi ya wanachama wa chama hicho, jana alifika mahakamani kusikiliza mwenendo wa mgogoro baina yake na Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ambapo baada ya kumalizika kwa kipindi cha mahakama, alipata fursa ya kuzungumza na waandishi wa habari. Akizungumzia sakata la madawa ya kulevya, Profesa Lipumba  alisema anaunga mkono suala la watuhumiwa wa dawa za kulevya, kukamatwa na kuongeza kuwa serikali inapaswa kuungwa mkono katika suala hilo.