Afrika Kusini yarejea nyuma katika azma yake ya kujiondoa mahakama ya ICC

0
62

Serikali ya Afrika Kusini imetangaza rasmi kuachana na azma yake ya awali ya kutaka kujiondoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Serikali ya Afrika Kusini imechukua uamuzi huo kwa kumtaarifu Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, baada ya mahakama kuu ya nchi hiyo mwezi jana kuitaka serikali iachane na mpango wa kujiondoa ICC. Katika taarifa hiyo serikali ya Pretoria imetangaza kuwa: “Kutokana na taarifa ya kabla iliyotumwa kwa Umoja wa Mataifa juu ya uamuzi wa kujiondoa ICC, uamuzi ambao ulizingatia vielelezo dhaifu na bila kufuata sheria, sasa Afrika Kusini inarudi nyuma katika suala hilo.”


Marais wa Afrika Kusini na Sudan wakionyesha urafiki wao

Wakati huo huo Ayesha Johaar, kaimu mshauri mkuu wa serikali  ya Afrika Kusini ametangaza kuitwa nchi hiyo na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kwa ajili ya kujieleza juu ya sababu ya Pretoria kushindwa kumtia mbaroni Rais Omar al Bashir wa Sudan alipotembelea nchi hiyo miaka miwili iliyopita. Itakumbukwa kuwa mwaka 2015 na baada ya serikali ya Afrika Kusini kulalamikiwa na ICC kwa kushindwa kwake kumkamata rais huyo wa Sudan, Pretoria ilitangaza azma yake ya kutaka kujiondoa kutoka mahakama hiyo.


Al-Bashir

Rais Omar al Bashir wa Sudan anatuhumiwa kuhusika na jinai za kivita na mauaji ya umati yaliyotokea nchini humo. Gambia na Burundi ni nchi nyingine zilizotangaza uamuzi wa kujiondoa mahakama hiyo kwa kulalamikia mienendo ya kibaguzi kwa kuwaandama viongozi wa nchi za Afrika pekee.