Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa zuio la muda kusitisha operesheni…..

0
38

DAR ES SALAAM

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imetoa zuio la muda kusitisha operesheni ya kuwaondoa kwa nguvu wananchi katika maeneo wanayoishi na kuwachomea makazi yao katika eneo la Loliondo wilayani Ngorongoro.

Tume hiyo imesema lengo la kufanya hivyo ni kulinda haki za pande zote. Taarifa ya Tume ya Septemba 4, iliyosainiwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga imesema hatua hiyo imechukuliwa kwa mamlaka iliyonayo kwa mujibu wa Ibara ya 130(1) (f) na (h) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Hatua hiyo amesema imefikiwa kutokana na tume kupokea malalamiko ya wananchi walioathiriwa na operesheni hiyo kutoka Tarafa ya Loliondo wilayani Ngorongoro.

Kwa mujibu wa taarifa za wananchi hao, katika operesheni iliyoanza Agosti 12 inayotekelezwa kwa pamoja na uongozi wa Wilaya ya Ngorongoro, askari wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti (Senapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na Jeshi la Polisi kumekuwepo na uvunjwaji wa haki za binadamu na misingi ya utawala bora.