IGP Sirro Ahaidi kuwasaka na kuwakamata wote waliousika kumshambulia Lissu

0
54

Jeshi la polisi limesema kuwa limemaanisha kwa dhati kuwasaka wahusika wa tukio la kushambuliwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kwa vile tukio hilo limewataajabisha wengi.

Inspekta Jenerali wa Polisi(IGP), Simon Sirro amesema katika hatua za awali tayari ametuma timu ya wapelelezi kwenda Dodoma kwa ajili ya kuongeza nguvu na kuwa upelelelezi huo utafanyika kwa umakini wa hali ya juu.

“Tumemaanisha na nataka niwathibitishie nyinyi waandishi wa habari kuwa jeshi la polisi liko imara na linafanya kazi yake imara. Lakini pia nataka muelewe hili tukio tumelichukulia ‘serious’ kwa umakini hivyo tuomba wananchi waendelea kutupa ushirikiano,” alisema.

Alidai kuwa hakuna haja kuanza kunyoosheana vidole au kulumbana juu ya nani yuko nyuma ya tukio hilo bali kinachopaswa ni kuunganisha nguvu kuwasaka watuhumiwa.

IGP Sirro amesea kama ilivyo kwa wengine naye ameona madai yaliyoibuliwa na Lissu kuwa alikuwa akiwindwa na watu fulani. Amesema maelezo yanayoendelea kuzunguka kwenye mitandao ya kijamii akionekana Lissu akimtuhumu yeye na kigogo wa usalama kwamba wamemtumia gari kwa ajili ya kumfuatilia siyo kweli.

“Lakini hili ni suala la hisia tu maana nimeona kwenye clip fulani anataja anasema Sirro…Kilifimba hii habari ya kusema, unajiuliza haya ambayo alikuwa anatishiwa ametoa taarifa kwa nani… ameripoti wapi, lakini siyo wakati muafaka wa kuanza kuulizana maswali wakati yeye akiwa hospitali suala msingi hapa amejeruhiwa amepigwa risasi tushirikiane,” amesema.

Amesema kuwa Lissu ni binadamu kama ilivyo binadamu wengine hivyo anaweza akawa na baadhi ya mambo ambayo majibu yake hayawezi kupatikana sasa mpaka hapo watakapokamatwa wahusika wake. “Huwezi kujua huko anakotoka huko anakokwenda lakini kikubwa zaidi tuwapate wahusika,” amesema.

Amesisitiza kuwa suala la ulinzi wa amani ni la kila raia kwani panapokosekana amani hiyo siyo mwanasiasa au muumini wa dini yoyote anayeweza kufanya mambo yake kwa uhuru. Siku moja tangu kutokea kwa shambulizi hilo kumekuwa na mkanda wa picha unaozunguka kwenye mitandao ya kijamii ukimwonyesha Lissu akiwa na waandishi wa habari na kudai kuwa amekuwa akiwindwa na watu wasiojulikana wanaotumia gari aina ya premio nyeupe.

Kwenye picha hiyo Lissu anasikika akisema “Ndugu zangu waandishi wa habari kabla sijaanza lolote naomba nitume salama kwa IGP Sirro na Kilifimba wa Usalama wa Taifa kuwa waache kuwatuma wale watu wanifuatilie…juzi nimewabana hapa St.Peters.” Akijibu swali kuhusu kutumika kwa silaha kubwa katika shambulio hilo la Lissu, Sirro amesema hilo siyo jambo la kushangaza kwa vile matukio ya kihalifu yamekuwa yakijitokeza mara nyingi na wahusika wake kutumia silaha za aina hiyo.

Katika hatua nyingine, IGP Sirro alizungumzia kuhusu hali ya usalama akisema vitendo vya uhalifu na ujambazi vimepungua na kuwataka wananchi waliokuwa na hofu ya kwenda maeneo ya Rufiji kuondoa hofu hiyo kwa vile jeshi hilo limedhibiti hali ya amani.

Kuhusu matukio ya utekaji watoto ambayo yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara katika siku za hivi karibuni, IGP Sirro amesema kwa kiasi kikubwa wale waliokuwa nyuma ya vitendo hivyo wametiwa mbaroni. “Haya matukio tayari tumeyadhibiti na wananchi wasiwe na hofu kwani baadhi yao tumewakamata bado tunaendelea na msako zaidi,” amesema.