Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa Augustine Mahiga afanya ziara Iran

0
45

Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa wa Tanzania, Augustine Mahiga anatazamiwa kuanza safari rasmi ya kikazi hapa nchini Iran leo Jumatano.

Bahram Qassemi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema Dakta Mahiga anatazamiwa kuongoza ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambao utakutana na kufanya mazungumzo na maafisa wakuu wa serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu masuala ya pamoja na kuimarishwa uhusiano wa pande mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania anatazamiwa kukutana na mwenzake wa Iran, Mohammad Javad Zarif na Rais Hassan Rouhani, pamoja na maafisa wengine wakuu serikalini hapa mjini Tehran.

Iran imekuwa ikisisitiza kuwa, kuimarishwa ushirikiano na uhusiano wa pande mbili katika nyuga za siasa, uchumi na utamaduni na nchi za Afrika ni katika ajenda kuu ya sera ya mambo ya nje ya nchi hii.


Waziri Mkuu wa Tanzania na Balozi wa Iran mjini Dar es Salaam, Moussa Farhang

Mapema Agosti mwaka huu, Maspika wa Bunge la Tanzania na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar walikutana na kufanya mazungumzo na Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran. ambapo walisistiza kuwa, kuimarishwa uhusiano wa makundi ya urafiki ya mabunge na kubadilishana tajiriba kunaweza kusaidia katika kuinua na kustawisha kiwango cha uhusiano wa nchi mbili.

Maspika hao wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania walikuwa hapa mjini Tehran kuhudhuria sherehe ya kuapishwa Dakta  Rouhani baada ya kuchaguliwa tena kuwa rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwezi Mei.