Serikali ya Burundi imekataa mpango wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) wa kutaka kuanzishwa uchunguzi wa jinai za kivita na ukatili uliofanyika nchini humo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Katika kikao na waandishi wa habari mjini Bujumbura hii leo, Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Aimee Laurentine Kanyana amesema serikali ya Bujumbura haitashirikiana na mahakama hiyo yenye makao makuu yake mjini The Hague nchini Uholanzi.

Amesema: “Tumesikia uvumi kwenye vyombo vya habari vya kimataifa kwamba ICC imetoa kibali cha kuanzishwa uchunguzi wa jinai na ukatili uliofanyika nchini Burundi, serikali haikubaliana na jambo hilo kabisa. Burundi ilijiondoa rasmi kwenye Mkataba wa Roma uliounda ICC Oktoba 26.” Mwisho wa kunukuu.

Jana Alkhamisi, majaji wa mahakama hiyo waliruhusu kuanzishwa uchunguzi kuhusu ukatili na jinai dhidi ya binadamu uliofanywa katika kipindi cha kati ya mwaka 2015 na 2017 dhidi ya raia wa Burundi ndani au nje ya nchi hiyo.


ICC: Watu 1200 wameuawa, maelfu wameswekwa jela kinyume cha sheria, maelfu wameteswa na mamia wametoweka

Jinai hizo ni pamoja na mauaji, ubakaji, ukatili na mateso yaliyoanza mwaka 2015 baada ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza kutangaza nia yake ya kugombea kiti hicho kwa muhula wa tatu mfululizo.

Hii ni katika hali ambayo, vyama vya upinzani nchini humo vimetangaza kuunga mkono mpango huo wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai. Charles Nditije, kinara wa jukwaa la upinzani la  CNARED ambaye yuko uhamishoni ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa: “Huu ni ushindi mkubwa kwa mfumo wa sheria nchini Burundi, na ni ushindi kwa wale wanaotaka kurejesha amani na utawala wa sheria nchini humo.”