DC HANDENI ATOA SIKU 14 WATAALAMU WA ARDHI KUAINISHA MPAKA UNAOTTENGANISHA HALMASHAURI YA WILAYA NA MJI KATA YA MISIMA.

0
20

Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe amewapa siku 14 wataalamu wa ardhi wa Wilaya kuainisha mipaka baina ya Kata ya Misima iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Halmashauri ya Mji ili kuondoa mkanganyiko wa mpaka uliodumu kwa muda mrefu.

Mkuu wa Wilaya ameyazungumza hayo jana alipokuwa kwenye mkutano wa Hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Msomera Kata ya Misima baada ya uongozi wa Kijiji hicho kuomba msaada wa kusikilizwa ili kuainishiwa mipaka baina ya Kata na Vijiji ili kuondoa muingiliano.

Mh. Gondwe alisema kuwa wataalamuwa ardhi watapima na kuonesha mipaka baina ya Halmashauri ya Mji na Wilaya ili wafahamu mipaka yao na kutambua wanapaswa kuitika wapi na kuondoa migongano inayokwamisha wananchi kushiriki katika maendeleo.

Alisema kuwa Msomera ni Kijiji kilichoanzishwa kisheria na kipo kwenye mpango wa matumizi bora ya ardhi hivyo wananchi wote wanapaswa kuheshimu na kufuata taratibu zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kuwataka wananchi wote wanaokuja kwenye Kijiji hicho na maeneo mengine  kufuata masharti ya maeneo husika kwani Tanazania ni huru kuishi kwa kila mwananchi isipokuwa kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Aliongeza kuwa Kijiji cha Msomera kilitengwa maalumu kwa mifugo, wakulima ambao walikuwepo kabla ya kijiji hicho kupangwa kuwa kwaaajili ya mifugo watambuliwe na hawataondolewa, wakulima waliokuja baada ya kijiji kutambulika kuwa ni cha mifugo wataondolewa.

Aidha Mkuu wa Wilaya amewataka wanakijiji cha Msomera kufuata utaratibu linapokuja suala la kuuza ardhi na kuingiza mifugo mipya kwa kushirikisha uongozi wa Kijiji na kufanya mikutano mikuu ya maamuzi ili kuwe na maaamuzi ya pamoja hata kama ardhi inayouzwa ni ya mtu binafsi.

“Kijiji kikipangiwa matumizi bora kitumike kama ilivyokusudiwa ili kuondoa  migogoro, tunzeni ardhi yenu na rasilimali zenu kwa ustawi wa vizazi vyenu,haijalishi kama mnaleta ndugu zenu, taratibu lazima zifutwe kinyume na hapo sheria itachukua mkondo wake” amesema Mkuu wa Wilaya.

 mmoja wa wafugaji akitoa malalamiko yake kuhusu wakulima kuvamia eneo la mifugo na kuanza kulima kinyume na taratibu na kuomba kuanishiwa mipaka kuepuka muingiliano.
 Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Handeni Bw.William Makufwe akiwaeleza wafugaji wa Kijiji cha Msomera kuwa  wakulima kuingia kwenye eneo la kufugia mifugo kunatokana na baadhi ya viongozi kutokuwa waadilifu kwa kuuza maeneo bila kufuata taratibu na kuwataka kushirikisha wananchi kwa kila jambo kwani viongozi sio watu wenye maamuzi ya mwisho.
 Kaimu  Mkuu wa Idara ya  Ardhi na Maliasili Bw. Napoleone Mlowe akithibitisha kuwa Kijiji cha Msomera kinatambulika kisheria na ni eneo lililotengwa kwaajili ya wafugaji kulingana na mpango bora wa matumizi ya ardhi.
 Mkuu wa Wilaya ya Handeni Mh.Godwin Gondwe akizungumza na wafugaji   wa Kijiji cha Msomera na akiwasisitiza kuwa Kuwa Kijiji hicho ni cha wafugaji wote bila kujali kabila.
Diwani wa Kata ya Misima Mh. Mariamu Killo akizungumza na wananchi wa  Kijiji cha Msomera na kuwataka kuwa wavumilivu hadi hapo mipaka itakapoainishwa.

Imetolewa na:
Kitengo cha Teknolojia, Habari na Mawasiliano
Halmashauri ya Wilaya ya Handeni
21/11/2017