Serikali imesema itaanza kutoa chanjo ya saratani ya shingo ya kizazi kwa wasichana kuanzia umri wa miaka 13, ifikapo Aprili, 2018 ili kupambana na ongezeko la ugonjwa huo Tanzania.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo Jumatatu Novemba 20,2017 wakati akipokea msaada wa vifaa vya uchunguzi wa awali wa saratani ya shingo ya kizazi na vifaa vya kufundishia kuhusu ugonjwa huo vyenye thamani ya Sh98 milioni.

Vifaa hivyo vimetolewa kwa Wizara ya Afya na wadau wa maendeleo kutoka Shirika la JhPiego kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (Usaid).

Akizungumzia msaada huo, amesema utaiwezesha Serikali kuendelea kupanua wigo wa huduma za uchunguzi dhidi ya ugonjwa huo. Waziri amesema takwimu zinaonyesha asilimia 80 ya wagonjwa hufika wakati ugonjwa ukiwa umefika hatua ya mwisho, hivyo kufanya matibabu kuwa magumu.