Licha ya kukiri kuwa hayakuwa matarajio yake, kocha mkuu wa klabu ya PSG ya Ufaransa Unai Emery, amesema timu yake kupangiwa kucheza na Real Madrid katika hatua ya 16 bora ya michuano ya klabu bingwa Ulaya ni kipimo tosha cha yeye kuonyesha uwezo.

Kocha Unai amewaambia waandishi wa habari kuwa, ili kuthibitisha ubora wake ni muhimu kukutana na timu bora, hivyo Madrid licha ya kuwa ni mabingwa watetezi ni saizi tosha kwa timu yake.

Katika droo hiyo iliyofanyika jana mjini Nyon nchini Uswisi, matokeo kuwa Juventus itacheza na Tottenham, FC Basel na Manchester City, FC Porto dhidi ya Liverpool na Sevilla wataikaribisha Manchester United nchini Hispania.

Kwingineo Shakhtar Donetsk itakuwa nyumbani kucheza na AS Roma, Chelsea watapambana na Barcelona na Bayern Munich watakuwa wenyeji wa Besiktas.

Mechi za raundi ya kwanza hatua ya 16 bora, zinatarajiwa kupigwa Februari 13,14,20, 21 na kurudiwa Machi 6,7,13 na 14.