Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametengua uteuzi wa walimu wakuu 31 wa shule za msingi wilayani Kiteto, ambao shule zao hazikufikia asilimia 50 ya ufaulu wa matokeo ya kuhitimu elimu ya msingi mwaka jana. Pia, Mnyeti ametengua uteuzi wa waratibu elimu wa kata 13 ambao shule zao hazikufikia asilimia 60 ya ufaulu na kuvunja kamati za shule hizo za msingi.

Wilaya ya Kiteto imeshika nafasi ya sita kati ya halmashauri saba za mkoa huo kwenye matokeo ya darasa la saba mwaka jana na kushika nafasi ya 168 kitaifa. Mkuu huyo wa mkoa alitoa uamuzi huo juzi kwenye siku ya kwanza ya ziara yake ya siku saba wilayani humo ya kujitambulisha, kukagua miradi ya maendeleo na kuzungumza na wananchi. Alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kiteto, Tamimu Kambona kujaza nafasi hizo baada ya waliokuwa wanazishikilia kuwashushwa vyeo.

Alisema walimu wakuu hao 31 na waratibu elimu kata 13 walishindwa kuwajibika ipasavyo kwenye nafasi zao hadi kusababisha wanafunzi wa shule hizo washindwe kufaulu. “Hao watakaoteuliwa kushika nafasi hizo nao watakuwa kwenye uangalizi hata katika muda wa wiki mbili au tatu, wakishindwa kazi tunawaondoa na kuweka wengine hadi tufike tunakokwenda,” alisema Mnyeti.