Jeshi la Misri limesema kuwa limeua magaidi wasiopungua 12 na kuwatia mbaroni wengine wapatao 100 katika opereseheni kubwa iliyoanzishwa na jeshi hilo kaskazini mwa Rasi ya Sinai.

Taarifa hiyo ya jeshi la Misri imetolewa leo Jumatatu, siku moja baada ya jeshi hilo kutangaza hiyo jana kwamba limeua magaidi 16 katika opesheni kama hiyo. Taarifa ya jeshi la Misri imeongeza kuwa ndege za kivita za nchi hiyo zimeshambulia maeneo 60 yakiwemo magari, maghala ya silaha na vituo vya mawasiliano vya magaidi. Jana Jumapili pia jeshi la Misri lilitangaza kuwa, limeua magaidi 16 kufuatia operesheni ya kijeshi katika eneo la Sinai.


Athari za mashambulizi na mapigano ya silaha katika Rasi ya Sinai, kaskazini mwa Misri

 

Taarifa ya jeshi la Misri iliyotolewa jana ilisema kuwa, washukiwa wengine 30 wametiwa mbaroni katika operesheni hiyo ya kijeshi iliyoanza katika Rasi ya Sinai tangu siku ya Ijumaa kwa amri ya Rais Abdul Fattah al Sisi wa nchi hiyo. Kwa miaka mingi sasa jeshi la Misri limekuwa likipambana na magenge yenye silaha katika Peninsula ya Sinai yaliyoshadidisha mashambulizi yao tangu jeshi la nchi hiyo lilipompindua Mohammad Morsi, rais wa kwanza kabisa kuchaguliwa kidemokrasia nchini Misri katikati ya mwaka 2013. Mwezi Novemba 2017, watu wasiopungua 235 waliuawa katika shambulizi la bomu na risasi lililofanywa na magaidi dhidi ya Waislamu waliokuwa wanasali katika msikiti wa mji wa Bir al Abed wa jimbo la Sinai Kaskazini huko Misri.

Jeshi la Misri limetoa wito kwa wananchi kushirikiana na vikosi vya ulinzi kwa ajili ya kuwaangamiza magaidi ambao wamekuwa wakihatarisha usalama katika Rasi ya Sinai. Makundi ya kigaidi yamekuwa yakifanya mashambulizi ya mara kwa mara katika Peninsula ya Sinai nchini Misri dhidi ya askari usalama, polisi na vituo vya ibada kama misikiti na makanisa.