Upande wa Mashtaka katika kesi ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inayomkabili mfanyabiashara, Ndama Hussein maarufu Pedeshee Ndama mtoto ya Ng’ombe, umeieleza mahakama kuwa wanasubiri nyaraka kutoka nchini Australia.

Ndama anakabiliwa na mashtaka matano ya kughushi na kujipatia dola 540,000 za Marekani kwa njia ya udanganyifu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu. Wakili wa Serikali, Estazia Wilson amedai leo Februari 12, 2018 mbele ya hakimu mkazi mkuu wa Mahakama hiyo, Victoria Nongwa, kuwa wameshapeleka maombi kwa ajili ya kupata nyaraka hizo.

Pia, wakili Wilson amedai kuwa mshtakiwa ni mgonjwa na leo ameshindwa kufika mahakamani hapo. “Mheshimiwa hakimu, tunasubiri nyaraka kutoka nchini Australia na mshtakiwa leo hajafika mahakamani kwa sababu ni mgonjwa, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajaa,” amedai.

Januari 10, 2018 kesi hiyo iliahirishwa baada ya upande wa mashtaka kuieleza mahakama hiyo kuwa wanasubiri nyaraka kutoka nchini Australia. Kuhusu nyaraka, wakili Wilson amedai kuwa wanazosubiri ni zile walizoomba kutoka nchini Australia. Hakimu Nongwa alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 28, 2018 itakapotajwa na dhamana ya mshtakiwa inaendelea

source:mwananchi