Tume ya Uchaguzi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imesema uchaguzi mkuu uliotazamiwa kufanyika Disemba mwaka huu 2018 hautafanyika bila mashine za kielektroniki.

Bila kutoa ufafanuzi wa kina, Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Uchaguzi ya Kongo CENI hapo jana alisema , “Hakuna uchaguzi Disemba 23 mwaka huu pasina mashine za kielektroniki za upigaji kura.”

Itakumbukwa kuwa, uchaguzi huo ulikuwa umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2016 na umeakhirishwa mara kadhaa kufikia sasa, kutokana na kile CENI inasema ni ukosefu wa fedha na maandalizi ya kilojistiki.


Corneille Nangaa, Mwenyekiti wa CENI

Mwishoni mwa mwezi uliopita, askari usalama wa Kongo DR waliwaua kwa kuwapiga risasi watu wasiopungua watano sambamba na kutumia gesi ya kutoa machozi kuvunja maandamano yaliyopigwa marufuku ya kumpinga Rais wa nchi hiyo Joseph Kabila, ambaye ameiongoza nchi hiyo kwa miaka 17 sasa.

Uamuzi wa Kabila wa kukataa kung’atuka madarakani baada ya kipindi chake cha uongozi kumalizika Desemba 2016 kimechochea maandamano kadhaa ya upinzani na kusababisha makumi ya watu kuuawa mbali na kushajiisha uasi wa makundi yanayobeba silaha katika maeneo mbalimbali ya nchi.