Mashabiki wa klabu ya Nacional De Montevideo ya Uruguay wameadhibiwa na shirikisho la vyama vya mpira wa miguu vya Amerika Kusini CONMEBOL, kutokana na kuwazomea wachezaji wa timu ya Chapecoense.

Katika mechi baina ya timu hizo mbili iliyofanyika Janauri 31, Mashabiki hao pia wanadaiwa kuwakejeli Chapecoense kwa kuimba na matamshi mabaya kuhusu ajali ya ndege iliyoua wachezaji wengi wa timu hiyo mwaka 2016.

Kutokana na makosa hayo, CONMEBOL jana imetoa uamuzi wa kuwafungia mashabiki hao kutohudhuria mechi tatu mfululizo za kimataifa timu yao ikicheza.

Katika hatua nyingine klabu ya Nacional imepigwa faini ya dola za kimarekani elfu themanini kutokana na vitendo vya mashabiki wake, licha ya kuwa Chapecoense walipendekeza CONMEBOL waifungie Nacional.